https://taifaleo.nation.co.ke/ KEG yatangaza tarehe za mjadala wa kuwaleta jukwaa moja wagombea urais mwaka 2022 Na CHARLES WASONGA MJADALA kati ya wagombea wa urais utafanyika Julai 12, 2022 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu baadaye Agosti 9, 2022. Awamu ya pili ya shughuli hiyo ambapo wagombea hao watapata fursa ya kufafanua sera zao kwa Wakenya, itafanyika mnamo Julai 26, siku 12 kabla ya siku ya upigaji kura. Akitoa tangazo hilo Jumatatu, Agosti 9, 2021 wakati wa warsha kuhusu maandalizi ya uchaguzi inayodhaminiwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipala (IEBC) katika mkahawa wa Flamingo, Mombasa, Rais wa Chama cha Wahiriri Nchini (KEG) Churchill Otieno aliwataka wagombea wa urais kujiandaa kwa mjadala huo. “Mjadala huu ni muhimu kwa sababu utatoa nafasi bora kwa wagombeaji urais kuelezea na kufafanua sera zao kwa umma. Shughuli hiyo itaandaliwa kitaalamu na wagombea watajibu masuala kuhusu manifesto kwa mpangilio bora,” akasema Bw Otieno. Akaongeza: “Kwa hivyo, tumeweka tarehe hizo kwa kuzingatia kwua wagombeaji urais watahitajika kuwasilisha karatasi zao za uteuzi kwa IEBC kati ya Mei 30 na Juni 10, 2022 kulingana na mwongozo ambao tayari umetolewa na tume hii.” Mtindo wa kuandaliwa kwa mjadala kati ya wagombea wa urais ulianzishwa nchini kuelekea uchaguzi mkuu wa 2013. Mjadala wa kwanza ulishirikisha wagombea wa urais wakati huo; Rais Uhuru Kenyatta, kiongozi wa ODM Raila Odinga na Musalia Mudavadi (ANC). Wagombeaji wengine wa urais wakati huo walikuwa Kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua, aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Elimu James Ole Kiyiapi, Mohammed Abduba Dida na Wakili Mkuu Paul Muite. Saba hao walijadili manifesto huku wakiangazia kuhusu changamoto zilizokuwa zikiisibu nchi hii wakati huo huku wakitoa mbinu za kukabiliana nazo. Katika uchaguzi mkuu ujao, wanasiasa kadha wameonyesha nia ya kutaka kumrithi Rais Uhuru Kenyatta ni pamoja na Naibu Rais William Ruto, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Bw Mudavadi, Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na Bw Odinga. Hata hivyo, kufikia sasa kiongozi huyo wa ODM hajatangaza rasmi kuwa atawania urais duru zikieleza kuwa atafanya hivyo mwishoni mwa mwezi huu wa Agosti. Aug 09, 2021 Tuanzebe ajiunga na Aston Villa kwa mkopo kwa mara ya tatu Na MASHIRIKA ASTON Villa wamemsajili upya beki Axel Tuanzebe wa Manchester United kwa mkopo wa msimu mmoja. Tuanzebe, 23, pia ametia saini mkataba mpya ambao sasa utamshuhudia akiendelea kuwa mchezaji wa Man-United hadi Juni 2023. Anarejea kambini mwa Villa kwa mara ya tatu muhula huu baada ya kuwajibikia kikosi hicho mara 35 katika kipindi cha miwili miwili ya mkopo kati ya 2018 na 2019. Beki huyo alikuwa sehemu ya kikosi cha Villa kilichopepeta Derby County kwenye mchujo wa kupanda ngazi hadi Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2019 ugani Wembley. Anarejea kambini mwa Villa siku chache baada ya kiungo na nahodha Jack Grealish kujiunga na Manchester City kwa Sh15.6 bilioni. Tuanzebe ni mchezaji wa tano kutua ugani Villa Park muhula huu baada ya Danny Ings, Leon Bailey, Emiliano Buendia na Ashley Young. Alijunga na Man-United akiwa na umri wa miaka minane pekee na amewajibishwa na miamba hao wa soka ya Uingereza mara 37 katika kikosi cha watu wazima tangu achezeshwe kwa mara ya kwanza mnamo 2017. TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO Aug 09, 2021 Isuzu EA yapangia Kipchoge mapokezi motomoto Na GEOFFREY ANENE KAMPUNI ya magari ya Isuzu East Africa imeeleza kufurahia balozi wake wa magari ya D-Max, Eliud Kipchoge aliyehifadhi taji la mbio za kilomita 42 kwenye Olimpiki 2020 nchini Japan mnamo Agosti 8. Kipchoge,36, alitwaa taji kwa saa 2:08:38 baada ya kuwa mbele pekee yake zikisalia kilomita 10. Mshikilizi huyo wa rekodi ya dunia ya wanaume ya umbali huo ya saa 2:01:39 kutoka ushindi wake wa Berlin Marathon mwaka 2018, amekuwa balozi wa magari ya D-Max tangu mwaka 2017. “Tunafurahi sana, kuvutiwa na kujivunia na mafanikio ya Kipchoge kwenye Olimpiki na pia kushirikiana naye. Imekuwa safari ndefu na inaendelea kuwa ya kusisimua. Tuna hamu ya kuendelea na ushirikiano huu hata zaidi,” kampuni hiyo imeambia Taifa Leo, Agosti 9, 2021 kupitia kwa afisa wake wa mawasiliano Dancan Muhindi. Alifichua kuwa kampuni hiyo inapanga kumuandalia mapokezi katika makao yake makuu yanayopatikana katika barabara ya Mombasa Road. Kufikia mwaka 2020, mfalme huyo wa marathon alikuwa amepokea Sh30 milioni kutoka kwa Isuzu East Africa ikiwemo kupewa gari la D-Max alipovunja rekodi ya dunia ya 2:02:57 iliyowekwa na Mkenya Dennis Kimetto katika Berlin Marathon mwaka 2014 na lingine mwaka 2019 alipoingia katika mabuku ya historia kwa kuwa binadamu wa kwanza kukamilisha mbio za kilomita 42 chini ya saa mbili. Alitimka mbio maalum za INEOS1:59 Challenge mwezi Oktoba 2019 kwa saa 1:59:40 jijini Vienna, Austria. Tangu isaini kandarasi na Kipchoge, kampuni hiyo inasema kuwa soko lake limeimarika kutoka asilimia 19 hadi 29 katika kipindi cha kwanza cha miaka mitatu. Kwenye Olimpiki 2020, Kipchoge alifuatiwa kwa karibu na Mholanzi Abdi Nageeye (2:09:58) na Mbelgiji Bashir Abdi (2:10:00), huku Mkenya mwingine Lawrence Cherono akikamata nafasi ya nne (2:10:02) naye Amos Kipruto alikuwa katika orodha ya wakimbiaji 30 ambao hawakumaliza. Kipchoge na Wakenya wenzake wanatarajiwa kuondoka Japan kurudi nyumbani mnamo Agosti 9. Huenda Kipchoge akaelekea nyumbani kwake mjini Eldoret katika kaunti ya Uasin Gishu kwanza kabla ya kurejea jijini Nairobi kwa mapokezi ya Isuzu East Africa. Nchini Japan, Kenya ilizoa medali ya dhahabu pia kupitia kwa Peres Jepchirchir (marathon ya kinadada), Emmanuel Korir (mita 800) na Faith Chepng’etich (mita 1,500). Hellen Obiri (mita 5,000), Ferguson Rotich (mita 800), Brigid Kosgei (marathon) na Timothy Cheruiyot (mita 1,500) walizoa medali za fedha nao Benjamin Kigen na Hyvin Kiyeng wakaridhika na nishani za shaba katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji. Polo aporwa na kisura ‘malaika’ Na JOHN MUTUKU SAMUEL HURLINGHAM, NAIROBI POLO alibaki kulia na kuomboleza kama mfiwa, akashindwa kutoka nje ya nyumba kichuna aliyemteka kwa ukarimu na urembo wake alipomuacha bila chochote. Jamaa alipokutana na mwanadada huyo hakufikiria anaweza kuwa hatari. Polo alihamia mtaani hapa majuzi baada ya kupata kazi yenye donge nono. Alipohamia mtaani, alikutana na kichuna aliyemdokezea aliishi karibu naye. Kichuna ndiye alimsaidia kupanga vitu katika nyumba, kazi ambayo polo hakuipenda. “Jamani sijui ingekuwaje iwapo usingetokea kunisaidia. Miye sijui kupanga vyombo vya nyumba,” polo alishukuru. “Usijali. Nipo kwa ajili yako. Bado napanga kukuletea maua bandia nikupangie huku na kule ila siwezi kwa kuwa sina ufunguo,” kichuna alisema. “Ufunguo huu hapa darling. Kila upatapo nafasi, kuwa huru kuingia humu mwangu,” polo alimhakikishia akimkabidhi ufunguo. Siku iliyofuata polo alipoenda kazini, kichuna alifika na vijana wake wanne. Walichukua kila kitu cha thamani katika nyumba hiyo, wakapakia katika lori kisha wakaondoka. “Mshenzi mkubwa huyo. Atokapo kazini atakuta atakayokuta,” kichuna alisemea akiondoka. Polo alipokuta nyumba ikiwa tupu, alijiinamia na kulia sana. “Laiti nisingalimkaribisha kwangu huyo mwanadada, haya yote yasingalinikuta. Hata hivyo, yaliyomwagika hayazoleki. Itabidi nisadiki nishatapeliwa na kichuna na nafaa kuwa makini,” polo alijiliwaza baada ya kuelezea majirani yaliyotendeka. Tangu siku hiyo, polo hapumbazwi na urembo wa mademu. Ameamua akitamani mke, itabidi amtafute kwa uangalifu. “Haufai kuamini mwanadada yeyote hii Kanairo. Ona sasa umepoteza mali kwa kuamini demu ambaye alijifanya malaika kwako ilhali humjui wala anakoishi,” jirani mmoja alimweleza jamaa.